ARUBAINI YA SUNGURA

na Yussuf Hamad


Hapo zamani za kale walikuwepo wanyama mbalimbali ambao waliishi kwa pamoja na kushirikiana kwa kila kitu. Siku mmoja Simba; mkuu wa wanyama aliitisha mkutano wa wanyama wote. Wanyama wote wailitikia wito.Siku ya kikao ilipofika wanyama wote walihudhuria katika mkutano huo muhimu wa wanyama. Simba alihutubia wanyama wote na kuwataka wachimbe kisima kwa sababu kulikuwa hakuna maji katika mito na maziwa. Wanyama wote walikubali rai hiyo ya mfalme Simba. Siku ilipofika wanyama wote walikutana na kuanza kuchimba kisima isipokuwa sungura tu. Sungura hakutaka kushirikiana na wanyama kuchimba kisima.Fisi alitumwa na mfalme simba akamuulize sungura kwanini hakuja kushiriki katika kuchimba kisima. Fisi alikwenda hadi nyumbani kwa sungura. Huko alimkuta sungura akiwa barazani akichambuwa karanga kwa ajili ya chakula chake cha mchana. Fisi alimsalimia sungura; ``Hujambo sungura?’’ Sungura alinyanyua uso wake na kumtazama fisi kisha akaitikia ``Sijambo fisi. Habari za siku nyingi?’’ Fisi nae aliitikia kwa kusema; ``Mimi sijambo pia! Ila tu nimetumwa nije kukuuliza kwa nini hujashiriki katika ujenzi wa kisima?’’ Fisi alimuuliza sungura.Sungura nae alicheka kidogo kisha akamwambia fisi; ``Mimi sina haja ya maji kwani nina maji yangu matamu sana. Maji mnayochimba yana matope na ni machafu. Mimi sipendi maji yenye matope. Nyinyi chimbeni kisima na mimi sitokunywa kamwe maji yenu hayo machafu!’’

Fisi aliondoka nyumbani kwa sungura na kuelekea kwa mfalme Simba. Alipofika alimweleza yote aliyoelezwa na sungura. Simba alisikitika sana aliposikia majibu ya sungura ambayo yalijaa kebehi na dharau kwa wanyama wengine. Lakini simba hakumchukulia sungura hatua yoyote. Baada ya siku kupita kisima kilimalizika na wanyama walianza kutumia maji. Kisima kilitoa maji mengi sana na wanyama wote walifurahi. Baada ya siku tatu tu tangu kisima kimalizike na watu waanze kuchota maji wanyama waligunduwa kitu amabacho si cha kawaida pale kisimani.
 Kila wakifika kisimani asubuhi waliona maji yamechafuliwa sana na kuingizwa takataka nyingi. Hivyo wanyama walimwambia Simba kuhusu uharibifu huu. Simba alifika kisimani siku iliyofuata na kuona maji yamechafualiwa sana. Simba aliamuwa kuweka ulinzi pale kisimani ili kumkamata anaeharibu maji. Hivyo zamu ya kulinda kisima ikapangwa. Mnyama wakwanza kuanza kulinda kisima alikuwa tembo. Tembo alilinda kisima usiku na alikuwa amejificha kichakani kumdoea mchafuzi wa maji kisimani. Ilipofika usiku wa manane, Tembo alisikia kiumbe fulani kinakuja. Tembo alikaa tayari kumkamata mchafuzi wa maji.Mnyama huyo alikuja hadi kisimani na alikuwa Sungura. Sungura alichota maji, kisha akakoga na baadae akaanza kuyachafua. Tembo alitoka kichakani na kumshika Sungura. Tembo alimwambia Sungura;``Leo nimekushika mchafuzi wa maji. Sikuachi hapa mpaka asubuhi nikupeleke kwa mfalme Simba ili ukapate adabu.’’ Sungura alicheka sana na kumwambia Tembo; ``Mimi sio muharibifu wa maji.Kwanza mimi sinywi maji haya. Maji haya si safi na wala si matamu. Mimi nina maji yangu matamu sana.’’ Sungura alitoa kichupa kidogo cha asali. Kisha akamwambia Tembo;`` Unaona haya ndio maji


ninayokunywa mimi. Haya ni matamu sana.’’ Tembo alishangaa sana na alimwambia Sungura tafadhali nionjeshe kidogo maji yako.’’ Sungura alimuonjesha Tembo ile asali ambayo alidai ni maji. Tembo alionja kidogo na kwa vile ilikuwa tamu alimwambia Sungura;’’ Tafadhali niongeze tena’’. Sungura alimwambia Tembo; ``Hapana! Siwezi kukuonjesha mpaka nikufunge katika mti kwani utanizidi nguvu na kuninyang’anya maji yangu matamu’’. Tembo alikubali na Sungura alimfunga Tembo katika mti mkubwa halafu akamcharaza viboko mpaka Tembo alikaribia kufa. Hapo sungura alimwambia Tembo nitakuachia lakini usimwambie mtu kuhusu mimi. Tembo alikubali na Sungura aliondoka na kumwacha Tembo akiwa amefungwa pale mtini. Asubuhi wanyama walipokuja walimkuta Tembo amefungwa amelala akiwa taabani. Walimuuliza kulikoni lakini tembo hakusema kitu. Siku iliofuata ilikuwa zamu ya Fisi. 
Nae alipata kipigo kama Tembo, kisha akaja punda ambae pia aliambulia kipigo. Wanyama wote waliopangwa walipigwa sana na Sungura.Akawa amebaki kobe. Kobe alimwambia Simba mimi nitaweza kumkamata mchafuzi wa maji. Wanyama wote walishangaa na kumwambia kuwa hataweza kwani wameshindwa wanyama wakubwa hivyo yeye hatoweza. Kobe alisema nitaweza na alikwenda kisimani. Alipofika alijipaka ulimbo mgongoni kwake. Sungura alipofika hakujua kuwa alikuwepo kobe hivyo aliona kuna jiwe tu pale kisimani. Sungura alipanda  juu ya mgongo wa kobe. Mara miguu yake iliganda.Sungura akasema; ``Umeikamata miguu yangu sio? Nina mikono pia’’. Sungura alipeleka mikono yake. Mikono ikanasa katika ulimbo na sungura akawa hawezi kutoka.asubuhi wanyama walipokuja walimkuta kobe akiwa ameganda mgongoni kwa kobe hana la kufanya. Kobe alimkabidhi sungura kwa samba kwa ajili ya kuhukumiwa. Wanyama wote walimpongeza Kobe kwa kazi yake nzuri.

4 comments:

  1. Kazi nzuri kwa wanafunzi wachanga.Itaweza kukuza vipawa vyao vya uandishi

    ReplyDelete
  2. nimefurahi sana nipikuwa naitaftaa xana🤣🤣

    ReplyDelete
  3. Hongera sana umetukumbusha mbali

    ReplyDelete